Sisi ni nani???

HISTORIA YETU

CASFETA ni jumuiya ya Wanafunzi mabalozi wa Kristo Tanzania iliyoanzishwa mwaka 1992. Wazo lake lilianzia kwa viongozi wa idara ya vijana wa TAG, yaani Christ’s Ambassadors (CAs). Aliyekuwa katibu mkuu wa CAs, Mchungaji Uswege Mwakisyala alikuwa ndiye mwenyekiti wa kamati ya watu watatu waliotengeneza mwongozo wa kwanza wa CASFETA. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Joseph Justine na ndugu Godfrey Mdoe. Lengo lilikuwa ni kupata chombo cha kuhudumia vijana waliookoka wa kipentekoste walioko mashuleni na vyuoni. Jina (CASFETA) yaani Christ’s Ambassadors Student Fellowship Tanzania lilibuniwa na Mchungaji ambaye sasa ni Askofu Uswege Mwakisyala. Jina hilo lina asili yake ni katika jina la idara ya Vijana ya kanisa la TAG....
Mwongozo huo alipewa Joseph Justine akiwa anafanya huduma ya wanafunzi na JUWAKWATA. Viongozi wa kwanza walikuwa kama ifuatavyo; Mwenyekiti alikuwa Doroty Mhando (Sasa ni Mrs D.Massawe yuko TAG Kinondoni), Katibu alikuwa Emanuel Akili na wajumbe wengine kama Elisha Joseph. Viongozi hao waliandika barua yao kwa askofu mkuu wa TAG tarehe 9/7/1992 kupitia kwa mkurugenzi mkuu wa CAs. Askofu mkuu wa wakati huo Mchungaji Ranwel Mwenisongole alijibu kwa barua yake ya tarehe 8/10/1992, kuikubali huduma hiyo ianzishwe na kusimamiwa na idara ya vijana CAs. Tarehe hiyo hiyo katibu mkuu aliandika barua kwenda wizara ya elimu ili kuitambulisha rasmi huduma ya wanafunzi.
Joseph Justine aliteuliwa kuwa mratibu mkuu akiwa mhitimu wa chuo cha biblia akifanya huduma chini ya Mchungaji Titus Mkama wa ilala TAG. Kwa nafasi yake kama mratibu mkuu aliandika barua inayoitambulisha CASFETA kwa taasisi mbalimbali nchini kuwa ni huduma inayodhaminiwa na kukulewa na kanisa la TAG. Mwaka 1993 mwongozo wa CASFETA wa kwanza ulibadilishwa ili kukidhi hoja ya kuifanya CASFETA ya wanafunzi wote wa makanisa ya kipentekoste.
Mwaka 1998 Joseph Justine aliasi maongozi ya TAG kisha akateuliwa mkurugenzi mpya wa CASFETA Mch. Mwakisyala kwa barua ya tarehe 16/11/1998 iliyopelekwa wizara ya elimu na kanisa la TAG ikiifahamisha wizara mabadiliko ya Uongozi. Baada ya uasi kutokea TAG ilimtenga ushirika wa kanisa mwaka 1998. Pamoja na changamoto hizo CASFETA iliendelea chini ya mkurugenzi mkuu Mch. Mwakisyala mpaka 2008 ikiwa na matawi zaidi ya 500. Mwaka 2008 CASFETA ilipata mkurugenzi mpya Mch. Dk, Huruma Nkone ambaye katika uongozi wake iliendelea kukua na kuzifikia shule, vyuo na vyuo vikuu vingi hapa nchini Tanzania. Kufikia mwaka 2020 kumekuwa na matawi zaidi ya elfu mbili mia tisa nchini kote.
Kwa sasa CASFETA inazidi kukua kwa kasi kubwa zaidi ikihudumia wanafunzi mbalimbali kutoka madhehebu ya kipentekoste nchini na kusimamia makusudi ya uwepo wake kama iliyoainishwa katika website hii. Ili kuendelea kukua katika dhamiri njema ya kuwalea wapentekoste wote mashuleni na vyuoni, Mwongozo wa CASFETA umeboreshwa sana na mpaka sasa CASFETA inatumia mwongozo wake toleo Rasmi la mwaka 2021.

Misingi yetu

01

MAONO

Kuwa kizazi kinachotembea katika nguvu za Roho Mtakatifu na kuubadilisha ulimwengu kwa Neno la Mungu.

02

MAADILI YA MSINGI

  • Uaminifu Kwa Biblia
  • Uadilifu kwa Jamii
  • Upendo na Mshikamano
  • kuvuna Kimkakati

03

MAKUSUDI YA CASFETA

Kuwawezesha wanafunzi kumwabudu Mungu kulingana na imani yao ya kipentekoste.

04

DHIMA

Kuwafikia wanafunzi wote kwa Injili ya Kristo kimkakati na kuwajenga kiroho kwa njia ya Kuabudu na Ushirika.

VIONGOZI WA CASFETA KITAIFA